Gospel Kitaa™
Wednesday, 19 June 2013
ANGALIA VIDEO ASKOFU KAKOBE AKIWA NCHINI CANADA NA WANAHABARI
Angalia video ya askofu Zachary Kakobe akiwa nchini Canada akizungumza na waandishi wa habari tayari kwa mkutano mkubwa wa injili "Toronto Miracle Healing Crusade" unaotarajiwa kuanza hapo kesho.
Tuesday, 18 June 2013
RON KENOLY NA DON MOEN KUMPA TAFU ASKOFU KAKOBE NCHINI CANADA ALHAMIS HII
Mwimbaji nguli wa muziki wa injili duniani Ron Kenoly anatarajiwa kuwa mmoja wa waimbaji watakaoimba katika mkutano mkubwa wa injili wa kimataifa ulioandaliwa na askofu Zachary Kakobe ambao unatarajiwa kuanza alhamisi hii tarehe 20 hadi 23/6/2013 katika uwanja wa Rexall Centre Tennis katika jiji la Toronto nchini Canada.
Waimbaji ambao tayari wametajwa kuimba katika mkutano huo ambao umepewa jina la "Toronto Miracle Healing Crusade"ni pamoja na nguli mwingine Don Moen, kundi la wanandugu Krystaal, Martha Munniz na waimbaji wengineo, mkutano huo utakuwa wa kwanza kufanyika katika uwanja huo wa tennis huku pia askofu Kakobe kupitia huduma yake ya BZKIM inafanya kuwa muhubiri wa kwanza kutoka Tanzania na Afrika mashariki na kati kufanya mkutano mkubwa sehemu ya wazi kama ilivyo kwa watanzania kushuhudia wahubiri wakubwa wakija kuhubiri nchini.
Wiki iliyopita askofu Kakobe alikaririwa akiwatoa hofu waumini wake kutokana na madai ya kwamba amewatoroka na kuwaambia kwamba anakwenda kutimiza agizo la Mungu kuhubiri Canada katika mkutano mkubwa tena akitumia lugha ya Kiswahili. Kama hukusoma BONYEZA HAPA.
HIVI MPENDWA ULIKUWA UNAJUA KUWA FEDHA AU MALI INA NGUVU KULIKO MOYO WAKO?
![]() |
| Pastor Carlos Kirimbai |
Andiko la Msingi ambalo Mtumishi huyu wa Mungu ambaye ninamwadmire sana alilitumia linapatikana kwenye kitabu cha Mathayo sura ya sita:
Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako. (MT. 6:19-21 SUV).
Mstari wa 21 ndipo yalipo maneno ya ufunguo:
".. kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako."
Ni wazi na ni dhahiri kutokana na maneno haya hazina au mali yako au fedha yako kwa maneno mengine ina nguvu ya kuuvutia moyo wako kule unapoipeleka. Pale unapowekeza fedha yako au mali yako, moyo wako upende usipende utavutika huko.
Kuna namna ambavyo Mungu ametuumba wanadamu kiasi kwamba tunapopeleka hazina yetu, mali zetu, fedha zetu, moyo wetu unavutika huko.
Neno lingine kwa ajili ya neno moyo ni neno nafsi. Kwenye nafsi hususa moyo kuna vitu vitatu:
1. Nia zetu ambazo kwazo tunafikiri na kukokotoa taarifa ambazo zinaingia ndani yetu kupitia milango mitano ya fahamu.
2. Utashi ambao kwa huo twafanya maamuzi.
3. Hisia ambayo kwa hiyo tunahisi kupenda au kuchukia, kufurahi au kusikitika nk.
Sasa kwa andiko hilo hapo juu kama ilipo hazina yetu ndipo utakapokuwepo na moyo wetu ina maana waziwazi kuwa kule tupelekako fedha na mali zetu itaathiri maamuzi yetu, kufikiri kwetu na hisia zetu.
Utajikuta tu hatimaye unaanza kuamua katika mwelekeo wa kile ambacho unawekeza, utaanza kujisikia kupenda na kufurahia kile ambacho unawekeza huko na utajikuta unashindwa kuacha kufikiria kile ambacho huku ndo unawekeza.
Mungu anashindwa kuacha kutupenda, anashindwa kuacha kutufikiria, anashindwa kuacha kufanya maamuzi kwa faida yetu maana amewekeza sana kwetu kwa njia ya kumtoa Mwanae wa Pekee kwa ajili yetu. Amesha wekeza mno kwa mwanandamu na ndo maana mwanadamu ni tunu ya jicho la Mungu. Ndo maana hata kama mwanadamu kakoseaje, katenda dhambi kiasi gani, akija kwa Mungu kwa unyenyekevu na kuomba msamaha anasamehewa mara moja maana Mungu kwa hazina aliyoitoa kwa mwanadamu moyo wake umevutwa kwa mwanadamu.
Ndugu yangu mpendwa unapoanza kuwekeza katika Ufalme wa Mungu kwa njia ya fedha zako ama mali zako, unapofanya hivyo kwa uamnifu, bila kujua moyo wako unaanza kuvutwa kumwelekea Mungu ambaye Ufalme Wake wewe unawekeza ndani yake. Unachokitoa kama sadaka kwa Mungu kinaanza kuuvuta moyo wako kumwelekea Mungu na itaathiri sana hisia zako kumwelekea Mungu, jinsi ambavyo unamfikiria Mungu na hatimaye maamuzi ambayo unayafanya kuhusu Mungu.
Ninakupa changamoto, embu anza kwenye kipato chako anze kuwekeza kwa Mungu uone itafanya nini kwa moyo wako. Hata kama unajihisi upo mbali kiasi gani toka kwa Mungu anza kuwekeza. Unatamani upendo wako kwa ajili ya Mungu uongezeke, anza kuongeza unavyowekeza kwa Mungu.
Kumbuka, pale ilipo hazina yako, ndipo utakapokuwepo na moyo wako.
Bila kuingia kinaga ubaga katika yale nitakayo yataja ngoja nikuorodheshee aina ya sadaka ambazo zinakubalika mbele za Mungu na nakuhakikishia utakapoanza kuzitoa huku ndani yako ukijua unamtolea Mungu, moyo wako utaanza kuvutwa kumweleka Mungu.
1. Malimbuko: Malimbuko ni sadaka ambayo kwa jina lingine inaitwa Cha Kwanza, Uzao wa Kwanza,mshahara wa Kwanza, faida ya kwanza, ongeo la kwanza, mavuno ya kwanza, maziwa ya kwanza, uzao wa kwanza wa mifugo yako nk.
Utaratibu wa utoaji wa sadaka hii kimaandiko ni kwamba inaenda kwa mtumishi wa Mungu. Kama kuna mahali una abudu basi ipeleke kwa Mchungaji wako na umwambie ni malimbuko naye atakuombea baraka sawasawa na neno linavyoagiza. Sasa ukipeleka usione kama unampa Mchungaji wako, bali ona kuwa unampa Mungu ila Mungu ameagiza katika neno Lake umpelekee kuhani wako au kwa maneno mengine Mchungaji wako.
Monday, 17 June 2013
UMASIKINI UMEMTAMBULISHA SANA YATIMA KULIKO UYATIMA WENYEWE.
Hezekia Mwalugaja - Mkurugenzi na m'beba maono wa Kituo cha Hananasif Orphanage Azungumza na Blog Hii(Mdee junior blog).
Mara nyingi unamtambua yatima kwa sababu anavaa vibaya, hali vizuri. Lakini yatima sio lazima avae vibaya au ale vibaya na hiyo sio tafsiri ya Yatima.
Tafsiri ya yatima ni kuondokewa wazazi lakini pia sio kufiwa wazazi.
Tuna watu katika ulimwengu tunaoishi wana jina la kuitwa yatima japo hawajapoteza wazazi (hawajafiwa).
Kwa hiyo kigezo kikubwa ni mazingira yanayomzunguka ndo utambulisho wa kwanza wa mwenye sifa ya kujiunga na shule hii ya HOCET ama kituoni Kinondoni. Hivyo anaweza kuwa amefiwa na wazazi au hakufiwa lakini ana maisha mabaya kuliko wanaoitwa wamefiwa na wazazi.
Ikiwa limebaki Juma moja kabla ya Lile Tamasha kubwa la kumsifu Mungu pamoja na Watoto wa Mungu kutoka kituo cha watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu kijulikanacho kama HANANASIF ORPHANAGE CENTER (HOCET), Blog hii leo tarehe 15-06-2013 Imetembelea kituoni hapo ''Mkuranga Base'' ( HOCET SECONDARY SCHOOL ).
LENGO LA TAMASHA HILI NI KUCHANGIA KITUO HIKI CHA WATOTO YATIMA_HOCET
Jambo la kwanza ambalo liliifanya blog hii istaajabu ni pale Mkurugenzi alipoonyesha jengo lenye vyumba vitatu vya madarasa ambalo lilijengwa kwa siku sita (usiku na mchana), I was like woooow!
Shule hii ilianza mwaka 2007 ikiwa na wanafunzi 40 na walimu wa 3, Lakini kwa sasa ina wanafunzi 100 na walimu 8. Shule hii inachukua wanafunzi wa imani zote. Watoto hawa wanapatikana kutoka nchi nzima kupitia Serikali (ustawi wa jamii) na makanisani ambako kuna huduma za ustawi wa jamii.
Mkurugenzi, Hezekia Mwalugaja aliendelea kwa kuelezea lengo la mfumo wa maisha hapo kituoni.
Namnukuu: '' Lengo la kubadili mifumo ya kuishi ni kwa sababu maisha ya watu ambao tunaishi nao ni yale ambayo yametoka kwenye maisha magumu. Hivyo ili kuwaondoa kwenye maisha magumu ni kuwajengea uwezo wa kubadilisha mazingira(environment) waliyozoea ili waishi kwenye maisha mengine ambayo yana matumaini ambayo yanajumuisha elimu (formal & informal education) na kuinua vipaji/vipawa vyao ili wasiishie kutegemea tu akili ya kufundishwa bali pia ya kuzaliwa nayo (TALENT)''.
Maelezo yafuatayo yalitokana na maswali kutoka kwa Blog hii na waandishi mbalimbali wa habari ( Tv na Magazeti ) kama vile Clouds Tv, Tbc, Wapo Radio, Gazeti la Nyakati, Tanzania Daima na Jibu la maisha ambao nao walikuwepo eneo la tukio.
Kituo cha HOCET-Mkuranga kina jumla ya watoto mia moja na kumi (110). Watoto 100 wanasoma hapo na wengine 10 wanahudumiwa kwenye kituo cha mjini (Kinondoni). Hadi sasa kituo kimeshatoa kidato cha nne mara tatu.
Historia fupi ya HOCET.
Kituo kilianza mnamo mwezi Disemba 2002 pale Hananasifu Kinondoni kipindi cha kuelekea Christmas kwa sababu hiyo ndipo likazaliwa wazo kwamba:
Kristo haji kwao waliokuwa na unafuu wa maisha bali kwao ambao hawamjui na hawana unafuu wa maisha ili nao ujio wa Kristo uwe sehemu yao.
Mungu hakutupa kutunza yatima kwa wakati huo bali kuzungumza na kanisa kuhusu kujali na kutunza yatima kwa sababu kanisa limeondoka kwenye wajibu na kuachia jukumu lake kwa NGO's. Lakini kabla ya kuliambia kanisa/mtu mwingine ilibidi sisi wenyewe tujifunze kwanza namna iliyo bora ya watoto yatima ili tuwe tumevaa viatu (kubeba jukumu) kabla ya kuhamasisha wengine.
Aliendelea kusema, tunawafundisha watoto kuishi maisha ya kiroho na kumtumaini Mungu ili watambue kuwa kuondokewa na wazazi wao sio sababu ya wao kuwa na maisha mabovu/magumu.
Aidha, alienda mbali zaidi na kusema; tumekusudia kuwapa elimu ambayo italeta majibu katika maisha yao. Pia lengo la kuwaweka katika shule ya bweni ni ili kwamba baada ya vipindi vya masomo ya kila siku darasani wasirudi mtaani (USWAZI).
Vyanzo vya mapato.
Alipoulizwa, Mwalugaja alisema;
Kituo cha HOCET kina vyanzo vikuu viwili vya mapato ambavyo ni:
i> Networking.
Huu ni muunganiko/mwitikio wa waumini wa imani ya Kikristo na wale wa imani nyingine isiyo ya Kikristo kwa maana ya Watanzania wenye nia moja, dhamiri moja na moyo mmoja kwa kuleta sadaka zao.
ii> Vipawa vya watoto (TALENT).
Tumeinua vipawa vya watoto kwenye eneo la uimbaji. Watoto walifanikiwa kurekodi albamu yao ya kwanza inayojulikana kwa jina la NAJA KWAKO ambapo kazi hii iliuzwa mnamo mwaka 2006 na kuingia mapato kwa ujumla wake zaidi ya shilingi za Kitanzania milioni ishirini ( 20Ml).
Pia uuzwaji wa albamu hii uliendelea kutengeneza network kwa watu wa ndani ya kanisa na nje ya kanisa kupitia ujumbe uliomo kwenye albamu hiyo.
Blog ilitaka kujua kuwa Mkurugenzi Mwalugaja alitaka nisikie nini na Watanzania wajue nini na wafanye nini kwa ajili ya kituo hiki.
Ndipo alipofunguka zaidi na kusema:
Watanzania tunalo tatizo la kufikiri kwamba hatuwezi. Tunataka.
Tunataka kujenga uwezo wa Watanzania mkiwemo ninyi (waandishi) kwamba tunaweza pasipo mtu wa pili (mfadhili kutoka nje).
Ili tusonge kama taifa ni lazima tujiamini kuwa tunaweza ili wanapotokea watu kutoka nje ya nchi au nje ya familia yako kukutegemeza (support), wawe wanakutegemeza kwa sababu kuna kazi unayoifanya sio wao wawe sababu ya wewe kuwa na kazi unayoifanya. (hakika niliipenda hii point).
Tunataka Mtanzania wa leo afahamu kwamba mambo anayoyafanya anaweza kufanya mwenyewe.Unajua hawa watoto huko mtaani wamefanywa kuwa hawawezi kitu, lakini sisi kama huduma tunasema wanaweza kitu.
Ni lazima tuwajengee mfumo wa kufikiri zaidi kwamba wanaweza kuliko walivyofikiri kwamba hawawezi. Na ili haya yote yaweze kufanikiwa yanahitaji vitendea kazi, umoja wa dhati na sio umoja wa kuzungumza tu. Aliongeza kusema kuwa gharama za kuendesha shule kwa mwezi ni takribani milioni 15 kwa mahitaji ya msingi.
Mtazamo wa kituo juu ya kuchangisha fedha (fund raising)
Sisi kama kituo hatuamini katika kuchangisha fedha sana kila mahali bali tunafanya kazi sana itakayoleta fedha sana kwa ajili ya kuendesha maono.
Hivyo basi, ombi la msingi kwa Watanzania ni ''KUUNGANISHA NGUVU'' kama Watanzani tuweze kujivunia vitu vyetu hatimaye tuseme hivi ni vitu vyetu, hii ni akili ya kitanzania / kiafrika na sio wageni.
Kwa hiyo msaada tunaohitaji kwa media na watu mbalimbali TUUNGANE PAMOJA kwamba tunaweza bila kujali ukubwa wa gharama. Tuseme tunaweza katika yeye atutiaye nguvu, hii itatusaidia kuwaonyesha watoto uhalisi wa maisha kwa vitendo.
Blog iliendelea kudodosa ni kazi zipi kituo kinafanya mbali na zilizotajwa hapo awali kuleta fedha za uendeshaji wa kituo.
Mwalugaja akaeleza;
Kituo kina eneo la kutosha kufanya miradi mbalimbali.
Hadi sasa kituo kina ng'ombe kumi wa maziwa lakini lengo ni kuwa na ng'ombe 25 na kusudi ni kuwafundisha watoto kuweza kuona fursa nyingi kutoka kwenye ng'ombe maana ni zaidi ya kupata maziwa na samadi. Pia kituo kina mradi wa kuku wa kienyeji ambapo tayari wameshanunua mashine kutoka China yenye thamani ya Dollar za Kimarekani 2000 ambayo tayari ipo kituoni na pia wameshaagiza mayai kutoka Malawi na Morogoro nayo tayari yapo kituoni na kazi ya kutotoa vifaranga imeshaanza.
Blog hii ilimalizia mahojiano na MkurugenzI, Mwalugaja kwa kutaka kujua nini changamoto kama kituo kwa ujumla wake.
changamoto: NAMNUKUU.
* Namna gani Watanzania wanaweza kukubali kubaki kwenye mambo tunayoweza sisi wenyewe zaidi ya kusema ni lazima wafadhili wapatikane, na hapo ndipo shida inapotokea kwa sababu wafadhili wao ndo wanataka watupe mashari lakini sio sisi tuwape masharti ya kile tunachokifanya na hii ndio changamoto kubwa ya ujumla.
Lakini kwa upande wa elimu; Idadi ya walimu tulio nao hailingani na vile tunavyohitaji kwa sababu hatuna bajeti inayokidhi kuongeza walimu. Sababu nyingine ni namna ya kupata chakula cha kutosha kulisha shule nzima ikizingatiwa kuwa hakuna mtoto hana mmoja anayelipa ada.
Miundo mbinu haijakamilika, huduma za afya ziko mbali sana na kituo hivyo kuna changamoto ya usafiri pia.
Changamoto nyingine ya msingi ni kwamba, Jamii iliyowaombea watoto nafasi ndio yenye huruma na watoto kusoma, lakini watoto wenyewe hawana bidiii ya kusoma kama tulivyotarajia na ile ambayo walezi waliitarajia. Tunajaribu kuikabili changamoto kwa kuwafanyia watoto ushauri na saikolojia kwa msaada wa walimu kutoka Chuo Kikuu cha DSM.
![]() |
| Mambo ya Hocet, Mungu anazidi kuwainua hatua moja hadi nyingine. |
![]() |
| Mkurugenzi wa Hocet bwana Ezekiel Mwalugaja akionyesha mchoro uliochorwa ukutani kuonyesha kituo hicho |
![]() |
| Wanafunzi wakijiandaa na mitihani kwakusoma ndani ya maktaba yao. |
![]() |
| Moja ya darasa la Hocet linavyoonekana kwa ndani. |
![]() |
| ndani ya maktaba ni busy sana wanafunzi wakijisomea. |
MCH GWAJIMA AKEMEA WACHUNGAJI WANAODAI FEDHA BAADA YA MAOMBEZI
Na Mwandishi wetu kutoka Ufufuo na Uzima.
Mchungaji Josephat Gwajima atolea maelezo swala la wachungaji wanaodai fedha baada ya maombezi. Akisoma kwa habari ya Gehazi 2Wafalme 5:1-27, Mchungaji Gwajima alisema,
"Napenda kusisitiza, kanisani Ufufuo na Uzima maombezi ni bure na hakuna malipo yoyote ambayo mtu atatakiwa atoe baada ya maombezi. Kila mtu ataombewa bure kama biblia inavyosema Mathayo 10:8, "Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure." Kwasababu hiyo basi, ikitokea mtendakazi yeyote wa Ufufuo na Uzima akikuomba fedha kabla au baada ya maombezi au ikitokea mtendakazi yeyote akakutajia matatizo au madeni yake kabla au baada ya kukuombea, mtu huyo hatufai kabisa Ufufuo na Uzima.
Nasisitiza tena, hata kama ndugu yako alikuwa amekufa akafufuka, au alikuwa mgonjwa akapona, hutakiwi kutoa kiasi chochote cha hela kwaajili ya maombezi hayo. Katika kanisa la Ufufuo na Uzima maombezi ni bure, hivyo basi, mtu yeyote au mchungaji wa ngazi yoyote awe P. Shepherd, Sp on training, Shepherd, Mp, Ap au Rp akikuomba fedha baada ya maombezi au kukutajia matatizo yake; tafuta jina lake na ngazi yake alafu nitumie ujumbe mfupi wa maneno kupitia namba hii +255 (0) 654808036. Na mimi nitalishughulikia swala hilo haraka iwezekanavyo"
Akimalizia Mchungaji Gwajima alisema, "Watumishi wa Mungu wengi wamejikuta katika laana kwasababu ya kudai fedha, lakini Kama vile Gehazi alivyopata adhabu ya ukoma uliokuwa kwa Naamani, ndivyo itakavyokuwa kwa watumishi wa Mungu wanaodai fedha baada ya maombezi."
Sunday, 16 June 2013
TAMANI SANA URAIA WA MBINGUNI.*sehemu ya pili*
![]() |
| Mtumishi Gasper Madumla. |
Bwana Yesu asifiwe…
Haleluya….
Karibu tuendelee pale tulipokuwa tumeishia katika fundisho letu.
Tuliona mfano mmoja wapo wa Stefano mtu aliyejaa Roho mtakatifu,
mtu aliyejaa Neema na uwezo,mtu aliyejaa hekima,
jinsi alivyotamani sana kufanyika raia wa mbinguni maana mtu huyu aliuona utukufu wa Bwana Mungu pamoja na Bwana Yesu ameketi katika mkono wa kuume wa Mungu,angali akiwa bado anaishi kama mwanadamu wengine kabla ya kuuwawa. Tazama hata kifo cha Stephano,
Biblia inasema ;
“ wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.” Matendo 7 :58
Nguo za Stefano ziliwekwa miguuni mwa Sauli,
Hii ina maana kuwa utumishi aliokuwa nao Stefano uliwekwa miguuni mwa Sauli ikiwa ni ishara ya kuendeleza upako aliokuwa nao Stefano,
Maana nguo za Stefano zilikuwa sio kama nguo tu za kawaida,Bali zilikuwa ni Upako/Utumishi aliokabidhiwa Sauli ambaye baadae kidogo tunamuona anatokewa na Bwana Yesu njiani kisha hata jina lake linabadilika na kuwa mtumwa wa Kristo Yesu,aliyeitwa kuwa mtume na kutengwa aihubiri injili ya Mungu.
• Maisha ya mkristo haswa ni maisha ya umilele baada ya maisha haya kupita.
-Mitume wa Bwana Yesu nao ni mfano mzuri wa watumishi waliokubali kupoteza maisha ya damu na nyama ili kupata uraia wa mbinguni
Karibu mitume wote waliuwawa kwa kuishindania Imani,
maana waliona maisha haya ya kawaida ni maisha yenye kuharibika tu,hivyo walitamani sana kuvikwa vazi la umilele.
Tazama mfano mmoja pale Herode aliponyoosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga.
Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro.
Sasa tazama
Bibila inasema katika MATENDO 12:5
“ Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake.”
Hawa watu wa kanisa walijawa na ujasiri wa namna yake usioelezeka.Kwa sababu sio rahisi kwa kukamatwa kwa mwenzao na kuuwawa kwa upanga,
kisha kukamatwa tena mwingine naye akipangiwa kuuwawa kwa upanga,Tena Kisha wao muda huo huo wakakutana wote na kuaanza kuomba ,
Hii inamaanisha kuwa hata wao waliona ni afadhali kuuwawa kwa ajili ya Kristo Yesu na kwa ajili ya injili,maana kilichomfanya Yakobo ndugu yake Yohana kuuwawa ni injili ya Bwana yesu,na kanisa hawakukoma kuomba mpaka Petro walipomuona kwa macho yao.
* Jambo moja tunalojifunza kupitia mitume wa Bwana Yesu ni kwamba walidhalau maisha haya yasiokuwa na maana kabisa na kutamani sana uraia wa mbinguni.
Mfano wa tatu.
Mtazame Paulo ambaye anasema kufa kwake ni faida.
Anasema
“ Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.” Wafilipi 1: 21
*Tamani sana uraia wa Mbinguni,ambapo kila kitu cha hapa duniani,yaani vile ambavyo havina utukufu kwa Bwana hivyo utaviona kama mavi,na ndivyo Paulo alivyoona
“ Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;”Wafilipi 3:8
• Hivyo basi utagundua kwamba wanafunzi wa Bwana Yesu Kristo,waliteswa na hata wengine waliuwawa wakiishindania IMANI maana walitamani sana kuishi pamoja na Mungu Baba Mbinguni.
Hawa wote waliona thamani ya maisha ya umilele katika utumishi wao waliokuwa wakiufanya.
• Ndio maana wakailinda IMANI waliyoipokea mara moja tu,kwamba wasiipoteze,wakaitetea na kuitunza IMANI waliyokuwa nayo mfano wa KITO CHA THAMANI.
Waliona maisha ya mbele,na wakatiwa nguvu kwa kile walichokiona,
Na ndio maana hata Bwana Yesu aliwapa wanafunzi wake mfano wa ufalme wa mbinguni akiufananisha na hazina iliyositirika.
RON KENOLY NA MAJESTY NDIO CHAGUO LA GK JUMAPILI HII
Chaguo la Gospel Kitaa kwa leo liko kwa mtumishi wa Mungu kutoka nchini Marekani, Ron Kenoly. Pamoja na kuwa katika lugha ya kiingereza, nyimbo zake hugusa wengi kwa kuwaponya, kuwainua mioyo na hata kuwarudisha kundini.
Pata wimbo wa Majesty kutoka kwake, Gospel Kitaa inakutakia Jumapili njema yenye amani na mafanikio kwa kila utakachopanga kufanya.
Subscribe to:
Posts (Atom)










